Monday, April 26, 2010
WAALIMU KUCHAPWA BAKORA NA SUNGUSUNGU KISA KUCHELEWA KWENYE KIKAO
Chama cha walimu Tanzania kimesema kitaishtaki serikali kufuatia tukio la walimu wanne kuchacharazwa bakora mbele ya hadhara na sungusungu kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao.
Chama cha walimu Tanzania, kimesema kuwa kimesikitishwa na tukio la kuwadhalilisha walimu kwa kuwacharaza bakora mbele ya hadhara.
Tukio hilo limetokea mkoani Shinyanga ambapo sungusungu waliwacharaza bakora walimu wanne akiwemo mwalimu mmoja mwanamke ambaye alikuwa ni mjamzito.
Walimu hao walicharazwa bakora kwa kosa la kuchelewa kwenye kikao cha walimu na wazazi.
Afisa mmoja wa umoja wa walimu mkoani Shinyanga alisema kuwa wamechoshwa na tabia za mamlaka za dola kuwacharaza bakora walimu na wanatarajia wahusika watafikishwa mahakamani.
Mwaka jana mkuu wa wilaya ya Bukoba, Albert Mnali alisimamishwa kazi baada ya kuwaamuru polisi wawachape bakora walimu 32 kutokana na matokeo mabaya ya mitihani ya darasa la saba.
Mkuu huyo wa wilaya aliamuru polisi mmoja kuwachapa viboko walimu katika shule tatu za msingi zilizo Bukoba, kutokana na wilaya hiyo kuwa ya mwisho katika matokeo ya darasa la saba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment