Kundi la Al-Qaeda linaloongozwa na Osama Bin Laden limetishia usalama kwenye kombe la dunia nchini Afrika kwa kuahidi kufanya shambulizi la kigaidi litakaloua mamia ya watu wakati wa mechi kati ya Marekani na Uingereza.
Kundi la Al-Qaeda limetishia kuwaua mamia ya watu watakaohudhuria mechi kati ya Marekani na Uingereza kwenye kombe la dunia nchini Afrika Kusini mwezi juni mwaka huu.
Kundi linalojiita Al-Qaeda in the Islamic Maghreb, limetoa taarifa kwenye website likisema kuwa watu wa kujitoa mhanga wakiwa na mabomu ambayo si rahisi kugundulika kwenye mitambo ya ulinzi, wako tayari kujilipua kwenye mechi kati ya Uingereza na Marekani kwenye uwanja wa Rustenburg juni 12 mwaka huu.
Kundi hilo liliweka taarifa hiyo kwenye tovuti inayoitwa "Mushtaqun Lel Jannah" (Njia ya kuelekea peponi).
"Al-Qaeda watakuwepo kwenye mechi za kombe la dunia", ilisema taarifa hiyo ya Al-Qaeda.
"Litakuwa ni jambo la kufurahisha sana wakati wa mechi kati ya Marekani na Uingereza ikirushwa live kwenye luninga wakati sauti ya mlipuko itakaposikika kwenye majukwaa na kuugeuza uwanja mzima juu chini", iliendelea kusema taarifa hiyo ya Al-Qaeda.
Uingereza na Marekani zipo kwenye kundi moja la C pamoja na Algeria na watapimana ubavu juni 12 kwenye uwanja wa King Bafokeng mjini Rustenburg unaochukua watazamaji 44,500.
Maafisa wa Marekani wamesema kuwa vitisho hivyo vya Al-Qaeda vinachukuliwa kwa uangalifu mkubwa katika kuhakikisha usalama kwenye fainali hizo za kombe la dunia zitakazochukua mwezi mmoja.
Maafisa wa usalama wa Uingereza wamekataa kusema chochote.
Mwezi oktoba mwaka jana, maafisa wa usalama wa Afrika Kusini walisema kuwa wamefanikiwa kulizima jaribio la shambulizi la kigaidi lililokuwa limepangwa lifanyike wakati wa fainali hizo.
Iliripotiwa kuwa maafisa wa Afrika Kusini kwa kushirikiana na maafisa wa Marekani walifanikiwa kuwatia mbaroni watu wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa Al-Qaeda nchini Somalia na Msumbiji ambao walikuwa wakijiandaa kufanya shambulizi wakati wa fainali za kombe la dunia.
Serikali ya Afrika Kusini imetangaza kuwa jumla ya polisi 44,000 watalinda usalama kwenye fainali hizo.