Sunday, March 28, 2010
SIMBA KUVUNJA REKODI YA MWAKA 1993
Wachezaji wa Simba wakishangilia ushindi katika mojawapo ya mechi za ligi kuu ya Bara Saturday, March 27, 2010 3:51 AM
MABINGWA wa Bara, timu ya Simba ya jijini Dar es Salaam wamepania kuvunja rekodi yao ya mwaka 1993 ya kufika fainali ya Kombe la CAF, ambapo sasa wanataka kutwaa taji la Shirikisho hilo la Afrika. Simba mwaka 1993 ilitolewa katika fainali za CAF baada ya kufungwa 2-1 na timu ya Stella Abdjan katika mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).
Katika mchezo wao wa kwanza, timu hizo zilitoka suluhu na hivyo Simba ilihitaji ushindi wa angalau bao 1-0 ili kutwaa taji hilo.
Meneja wa timu hiyo, Innocent Njovu alisema jijini kuwa wana uhakika wa kutwaa taji hilo kutokana na kuwa na kikosi bora kama cha mwaka 1993.
Njovu alisema mbali na kikosi hicho kuwa bora pia wachezaji wao wamekuwa na ari ya ushindi baada ya kutwaa ubingwa wa bara mapema kabla ya ligi kumalizika, wakiwa wamesaliwa na mechi mbili kibindoni.
"Sisi tuna uhakika wa kufika kwenye fainali kwani kwa sasa kikosi ni bora, na wana ari ya kushinda katika kila mechi wanayocheza, hivyo kutokana na dhamira hiyo tuna uhakika wa kufikia hatua ya juu zaidi yaani ya fainali," alisema Njovu.
Alisema baada ya kuwapa mapumziko mafupi wachezaji wao, watapiga kambi huko Zanzibar kujiandaa na mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Lenghten ya Zimbabwe.
Katika mchezo wa awali uliofanyika Zimbabwe Ijumaa iliyopita, ambao Simba iliyofuzu hatua ya pili moja kwa moja, waliwashinda wapinzani wao kwao kwa magoli 3-0, ushindi ambao ni mnono kwa klabu hiyo.
Hata hivyo, Njovu alisema wapinzani wao sio wa kubeza kutokana na kandanda safi waliyoionyesha na wanaamini mchezo wa marudiano utakaofanyika Jumapili ijayo jijini Dar es Salaam, utakuwa wa ushindani mkubwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment