Thursday, April 8, 2010
MAALIM SEIF SHARIF AANDIKA HISTORIA MPYA ZANZIBAR
MILANGO ya mwafaka inazidi kufunguka visiwani Zanzibar, baada ya Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad kwa mara ya kwanza tangu afukuzwe CCM, kuingia makao makuu ya chama hicho Kisiwandui kulikofanyika dua ya kumwombea rais wa kwanza wa Zanzibar, Hayati Abeid Amani Karume.
Dua hiyo ilifanyika jana katika Ofisi Kuu ya CCM, Kisiwandui, mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali ya Zanzibar na ya Jamhuri ya Muungano, mabalozi, viongozi wa dini na madhehebu mbalimbali.
Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 20 kwa Maalim Seif kuingia kwenye jengo hilo la CCM tangu afukuzwe uanachama wa chama hicho mwaka 1988.
Akizungumza na waandishi wa habari, muda mfupi baada ya dua hiyo, Seif alisema uamuzi wake wa kushiriki ibada hiyo umelenga kuonyesha kuwa uhasama wa CUF na CCM uliodumu kwa muda mrefu, umemalizika.
Alisema CUF wanautambua mchango mkubwa uliotolewa na mwasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 katika kuijenga Zanzibar imara na yenye umoja.
“Mzee Karume ndiye aliyeuanzisha msingi wa umoja Zanzibar. Na sisi sasa tunafuata nyayo zake katika kuimarisha umoja, maelewano na mshikamano kwa Wazanzibari wote,� alisema Maalim Seif.
Maalim Seif alisema ushiriki wa CUF katika sherehe hizo ni muelekeo mpya wa kuijenga Zanzibar ambapo sasa tafauti za kisiasa zinabakia kwenye sera na itikadi za vyama.
"Uhasama sasa uko kwenye sera na itikadi, lakini, linapokuja suala la kitaifa kama hilo, sote tunabakia kuwa Wazanzibari kwanza, vyama vyetu baadaye,�alisema.
Akizungumza katika dua hiyo, kwa niaba ya Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Mufti Mussa Salim, aliisifu picha iliyojitokeza hapo ya umoja na mshikamano wa Wazanzibari na akaomba iendelee kudumishwa.
“Marehemu Mzee Karume alisimamia umoja wa Wazanzibari. Na mtoto wake (Rais Amani Karume) leo hii anavaa viatu vya baba yake kwa kuwaunganisha Wazanzibari. Tunamuona Maalim Seif kaja hapa kuunganika na ndugu yake katika kukumbuka kifo cha mzee wao. Huu ndio umoja unaotakiwa,� alisema Sheikh Salim.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Katoliki, Jimbo la Zanzibar Augustine Shao, alisema kwamba historia ya Zanzibar haiwezi kuzungumzia maendeleo ya visiwa hivi bila kumtaja na kumtukuza Marehemu Mzee Karume, kwani ni kutokana na busara, ubunifu na kipaji alichojaliwa kiongozi huyo na Mwenyezi Mungu, ndio maana Zanzibar imefika ilipofika.
Tokea kufikiwa kwa maridhiano baina ya vyama vya CCM na CUF hapo Novemba 5, 2009, kumekuwa na matukio kadhaa ambapo Maalim Seif na Rais Karume wamekuwa wakikutana katika shughuli za kijamii na kimaendeleo, jambo ambalo hapo nyuma halikuwa likifanyika kutokana na mivutano ya kisiasa.
Juzi Rais Karume alijumuika na waalikwa wengine katika hafla ya harusi ya binti wa Maalim Seif huko Bwawani, mjini Zanzibar, tukio ambalo limezidisha mahusiano ya karibu ya viongozi hao na wafuasi wao.
Baada ya kisomo hicho cha hitima ambacho hufanyika kila Aprili 7, viongozi hao na wananchi walimwombea dua, marehemu Abeid Karume katika kaburi lake lililopo pembezoni mwa afisi hiyo ya CCM Kisiwandui iliyoongozwa na viongozi wa dini mbalimbali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.
Aidha, mjane wa Mzee Karume, Mama Fatma Karume, alishiriki katika hitima hiyo akiongozana na mke wa Rais wa Zanzibar Mama Shadya Karume na mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Salma Kikwete na viongozi wengine wanawake wa kitaifa wakiwemo Mawaziri, wabunge, wawakilishini na wananchi kutoka sehemu mbalimbali ya Zanzibar na Tanzania Bara.
Aprili 7, 1972 ndiyo siku aliyouawa Rais wa Kwanza wa Zanzibar marehemu Mzee Abeid Amani Karume na wapinga maendeleo nchini.
Wakati huo huo, Rais Kikwete amekata mzizi wa fitina na kutoa msimamo wa CCM juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar.
Kauli ya Rais Kikwete imekuja siku chache baada ya baadhi ya wana CCM kupita matawini na kueneza uvumi kwamba msimamo wa chama chao juu ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa haujatolewa rasmi.
Mbali ya wana-CCM kupita katika matawi pia wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa upande wa CCM katika kikao kilichomalizika wiki hii waligomea kuuchangia mswaada wa kura ya maoni juu ya uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa wakidai kwamba hawajasikia msimamo wa chama juu ya suala hilo.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya kifo cha marehemu Mzee Karume yaliofanyika viwanja vya Maisara Mjini Unguja Rais Kikwete alisema msimamo wa chama ni kuunga mkono uundwaji wa serikali ya umoja wa kitaifa.
Hata hivyo, aliwataka vijana kujitokeza kwa wingi katika kupiga kura ya maoni juu ya uundwaji wa serikali hiyo kwani faida zake ni nyingi kuliko hasara.
Alisema serikali ya umoja wa kitaifa ndio yenye maslahi kwa wananchi wa Zanzibar ambayo itavunja mambo yanayojitokeza kila wakati wa uchaguzi pamoja na kuondoa chuki na uhasama miongoni mwa Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Alisema uamuzi huo umepitishwa na CCM hivyo hauna matatizo wala shaka yoyote na azimio hilo lilitokana na kikao kilichofanyika Butiama.
Aidha, Rais Kikwete alisema anajua kwamba kuna hisia na mitazamo tofauti juu ya suala hilo na baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha ukweli juu ya dhana nzima ya kuwepo kwa serikali ya umoja wa kitaifa, lakini msimamo wa chama ni kwamba umefika wakati suala hilo lazima lifanyike kwa kuwa litasaidia kwa kiasi kikubwa kujenga jamii bora.
Alisema uamuzi kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa haukuwa uamuzi rahisi kufikiwa kwa upande wa CCM hata kwa CUF, lakini alitumia msemo wa Kiswahili usemao ‘lisilobudi hutendwa’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment