WELCOME TO TANZAMERICA'S WORLD

Tanzamerica
Is a social network page that updates you with current news from Tanzania , America and around the world. Also, gives you the opportunity to link up your business or ministry between Tanzania and America .We are also dealing with Entertainments (music,movie and art) news, and sports between the two country.
For more info on how to advertise your business, ministry, career and news
Contact us:
+1360 561 6629
Patrick.
tanzamerica@gmail.com
info@patricknworld.com
http://www.tanzamerica.blogspot.com
Detailed Info

http://www.celebafrica.blogspot.com
http://www.patricknworld.blogspot.com
http://www.reverbnation.com/patricknewman

Sunday, May 23, 2010

VIDEO - Wanaume Waliooana Malawi Watupwa Jela Miaka 14


Wanaume wawili wa nchini Malawi ambao waliiga tamaduni za watu wa magharibi na kuamua kuoana na kufanya sherehe kubwa, wamehukumiwa kwenda jela miaka 14 pamoja na kufanyishwa kazi ngumu.
Akitoa hukumu jaji wa mahakama ya Blantyre, Nyakwawa Usiwa-Usiwa alisema kuwa anatoa hukumu kali ili kuwalinda wananchi na watu wenye tabia kama ya wanaume hao waliooana.

Steven Monjeza, 26, na Tiwonge Chimbalanga, 20, walitupwa jela tangia walipotiwa mbaroni mwezi disemba mwaka jana wakati walipofanya sherehe ya harusi yao.

Kukamatwa kwa Monjeza na “mkewe” Tiwonge Chimbalanga kulisababisha Malawi iingie kwenye mgogoro mkubwa na mataifa ya magharibi ambayo yanatoa msaada kwa Malawi. Uingereza ambayo ndiyo mfadhili mkubwa wa Malawi iliweka wazi kukasirishwa kwake na kesi hiyo lakini haikusitisha misaada yake.

Mahakama ilijaa mamia ya watu na wengine walijaa nje ili kujua hukumu ya Monjeza na mwenzake. Walipotolewa mahakamani kupelekwa jela kuanza kutumikia vifungo vyao, baadhi ya watu walipiga kelele na kuwatupia maneno ya kejeli.

“Mmepata mlichostahili”, “Miaka 14 haitoshi ilibidi mfungwe jela miaka 50”.
Akiongea wakati wa kutoa hukumu, Jaji Usiwa-Usiwa alisema “Nitawapa hukumu ya kutisha ili kuilinda jamii na watu kama nyinyi na iwe mfano kwa wengine”.

Wakili wa washtakiwa aliitaka mahakama itoe adhabu ndogo kwakuwa vitendo vya Monjeza na mwenzake havimdhuru mtu mwingine yeyote.

“Ni watu wawili watu wazima ambao wanafanya mambo yao kwa siri. Hakuna mtu atakayedhurika iwapo wataruhusiwa kurudi kwenye jamii”, alisema wakili huyo.

Nayo taasisi ya kutetea haki za binadamu ya Cedep ya nchini Malawi, ilisema kuwa leo ni siku mbaya sana kwa Malawi.

“Inakuwaje wafungwe miaka 14 eti kwakuwa wanapendana? Hata kama wakifungwa jela miaka 20 jinsia zao haziwezi kubadilika”, mwanaharakati wa taasisi hiyo.

Jaji Usiwa-Usiwa alisema kuwa wanaume hao hawakuonyesha dalili yoyote ya kujutia tabia yao mbaya ya Sodoma na Gomora.

Wakati huo huo Marekani imelaani hukumu iliyotolewa na imesema kuwa hukumu hiyo ni hatua moja nyuma katika kulinda haki za binadamu.

Chini ni VIDEO ya Monjeza na mkewe mahakamani jana.


VIDEO - Wanaume Waliooana Malawi Watupwa Jela Miaka 14

Ajisalimisha polisi baada ya kutupa mtoto

JESHI la Polisi Mkoani Pwani, linamshikilia Eliza Mwalongo [20] aliyetupa kichanga mwenye umri wa siku tano mwishoni mwa wiki iliyopita huko Kibaha Kwa Mfipa.
Msichana huyo alitupa kichanga hicho njiani Mei 14 , mwaka huu, majira ya saa 12 asubuhi, na kumfunika kwa majani na miba na kilionekena na wapita njia waliopita katika njia hiyo na kutoa taarifa kituo cha polisi.

Baada ya kupatikana kwa taarifa hiyo kituo cha polisi msichana huyo aliamua kujisalimisha mwenyewe katika ofisi ya Serikali ya Mtaa wa Kwa Mfipa na baadae kupelekwa kituoni kwa mahojiano zaidi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Bw. Absaloom Mwakyoma amesema msichana huyo anahojiwa na baadaye atapelekwa kwa daktari ili akapimwe akili zake kama ziko sawasawa na mara baada ya uchunguzi msichana huyo atafikishwa mahakamani.

Msichana huyo alikuwa ni msichana wa kazi za ndani kwa Meja Mstaafu Lekule ambaye alikuwa akimfanyia kazi za mstaafu huyo lakini alikuwa akiishi kwake.

Kamanda alisema msichana huyo alitokea nyumbani kwao Iringa kuja kutafuta maisha ambapo tayari alishakuwa na mtoto mmoja ambaye alitengana na baba yake baada ya ugumu wa maisha ndipo alipokuja huku na kukutana na mwanaume aliyemzalisha na kuishi nae lakini alimkataa baada ya kuzaa mtoto huyo.
.
Kamanda Mwakyoma amesema kuwa, alipoulizwa ni kwa nini aliamua kufanya kitendo hicho alijitetea kuwa alifikia uamuzi huo kutokana na ugumu wa maisha unaomkabili kwa kuwa alikataliwa na mwanaume aliyemzalisha mtoto huyo.

Pia alisema asingeweza kumuhudumia mtoto huyo kwa kuwa tayari ana mtoto mwingine mdogo mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu na hakuwa na ndugu yoyote wa kumsaidia.

Kichanga hicho cha kiume kilizaliwa Mei 10, mwaka huu, na kimechukuliwa na hospitali ya Tumbi na kinaendelea vizuri.

MTOTO YATIMA AJARIBU KULIPUA UBALOZI WA MAREKANI DAR

MWANAFUNZI Nassib [16] anayekabiliwa na tuhuma za kutaka kujaribu kulipua ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam uchunguzi umebaini kuwa ni yatima anaishi na shangazi yake Kinondoni Moscow.
Habari hizo za uhakika kutoka ndani ya jeshi la polisi, zimebaini hilo na mwanafunzi huyo anaishi na shangazi yake aitwae Chiku Simba baada ya wazazi wake kufariki.

Imefahamika kuwa mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda umekuwa ukitumia watoto yatima, watoto wa mitaani na wajane kuwatumia kufanya vitendo vya ugaidi.

Hata hivyo shangazi yake alishangaa kutokana na kitendo hicho na alisema ameshitushwa na taarifa alizozipata kutoka kwenye vyombo vya habari kwa kuwa mtoto wake huyo hakuwa na vitendo vya kihuni na vya ajabu na majirani walithibitisha kuwa mwanafunzi huyo alikuwa ni mkarimu na hakuwa mtu wa makundi na hana tabia ya kukaa vijiweni.

Hata hivyo kati ya wanafunzi nane waliokamatwa juzi na maafisa wa polisi waliounganishwa katika tuhuma hizo saba wameachiwa huru na mmoja ambaye ni Amani Thomas anaendelea kushikiliwa kwa kuwa yeye ndiye aliongozana na Nassib hadi katika jengo hilo la ubalozi .

ATAKA TAKA KISA ATAKA KUPIGWA NA MME WAKE


Mwanamke mmoja nchini Iran amemfikisha mumewe mahakamani akidai talaka kwakuwa mume wake hajawahi kumpiga hata siku moja.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 24 [jina kapuni] alifungua kesi katika mahakama ya masuala ya familia mjini Tehran akilalamika kuwa mumewe hampigi hivyo anataka apewe talaka.

Kwa mujibu wa gazeti moja la kila siku la nchini Iran, mwanamke huyo aliiambia mahakama "Mume wangu ananitumikia na kunitunza vizuri sana lakini mimi nataka awe ananipiga, kama hawezi basi naomba anipe talaka yangu".

Mume wake ambaye ana umri wa miaka 28 alijitetea mahakamani "Mke wangu nampenda sana, sioni sababu ya kumpiga au kutumia maguvu dhidi yake".

Kwakuwa mwanamke huyo alisisitiza kuwa anataka awe anapigwa na mumewe au la apewe talaka, mahakama ilimruhusu mumewe awe anamshushia kipigo mkewe siku moja moja ili kuilinda ndoa yake.

Mumewe kwa shingo upande alikubali na aliahidi kuwa atakuwa akimshushia kipigo mkewe ili kumridhisha.

VIDEO - Panya Ndani ya Ikulu ya Obama


Hotuba ya Rais Barack Obama wa Marekani iliingiliwa na kitu asichokitegemea baada ya panya kukatiza mbele yake wakati akitoa hotuba ndani ya ikulu ya Marekani.
Rais Barack Obama alikuwa akitoa hotuba kwenye bustani maarufu ya Rose Garden iliyopo mbele ya ikulu wakati panya alipojitokeza na kukatiza mbele yake toka upande mmoja kwenye upande mwingine.

Wapiga picha waliokuwepo eneo la tukio hawakupitwa na panya huyo na walifanikiwa kuchukua taswira wakati kiumbe hicho kilipokuwa kikipita mbele ya mkuu wa taifa kubwa duniani.

Haijajulikana kama rais Obama alimuona panya huyo au la kwani alielendelea na hotuba yake bila kutetereka.

Taarifa zinasema kwamba panya huyo alionekana pia akipiga misele kabla ya Obama hajaanza kutoa hotuba yake.

Chini ni VIDEO ya tukio hilo.


VIDEO - Panya Ndani ya Ikulu ya Obama

Tuesday, May 18, 2010

ATUPWA JELA MAISHA YAKE YOTE BAADA KUMPASUA TUMBO MWANAMKE MWEZIE KWA LENGO LA KUCHUKUA KICHANGA


Mwanamke wa nchini Marekani ambaye alimlaghai mwanamke mjamzito na kumpeleka nyumbani kwake kabla ya kulipasua tumbo lake kwa kisu kwa nia ya kuiba kichanga chake, amehukumiwa kifungo cha maisha jela.
Mwanamke wa nchini Marekani ambaye alikuwa na shauku ya muda mrefu ya kuwa na mtoto, amehukumiwa kwenda jela maisha baada ya kuiba kichanga toka kwenye tumbo la mwanamke mjamzito.

Andrea Curry-Demus, 40, alipatikana na hatia ya kumuua mwanamke mjamzito Kia Johnson, 18 baada ya kulipasua tumbo lake na kisha kuiba kichanga kilichokuwa tumboni mwake na kujifanya yeye ndiye aliyejifungua kichanga hicho.

Curry-Demus akisomewa hukumu yake aliigeukia familia ya Kia na kuwaambia "Naomba mnisamehe".

"Naiomba radhi familia yake", alisema Curry-Demus kabla ya kumgeukia jaji na kusema "Nimekosa".

Mama yake Kia, Darlene Lee, aliridhishwa na hukumu iliyotolewa ya kifungo cha maisha jela akisema kuwa hakutaka Curry-Demus ahukumiwe adhabu ya kifo kwakuwa anataka ateseke kwa uovu alioufanya.

"Nataka ateseke na aione sura ya mwanangu kila siku anapoamka, afikirie kitendo alichofanya".

Hili si tukio la kwanza la Curry-Demus kujaribu kuiba kichanga toka kwenye tumbo la mwanamke mjamzito, miaka 20 iliyopita, Curry-Demus alihukumiwa kwenda jela miaka 10 baada ya kumchoma na kisu tumboni mwanamke mjamzito akiwa
na nia ya kulipasua tumbo lake na kuiba kichanga chake.

Katika tukio la hivi karibuni Curry-Demus aliiongopea familia yake kuwa yeye ni mjamzito baada ya kumlaghai Kia na kujifanya rafiki yake.

Alikuwa akitamba kwa marafiki zake kuwa yeye ni mjamzito akiwaonyesha picha ya Ultrasound aliyoiiba toka kwa Kia na kisha kuibandika jina lake.

Baada ya kutimiza azma yake ya kuiba kichanga cha Kia, aliiambia familia yake kuwa amejifungua mtoto kabla ya muda wake ingawa vipimo vya hospitali havikuonyesha kama aliwahi kuwa mjamzito.

Alitiwa mbaroni baada ya maiti ya Kia kugundulika nyumbani kwake baada ya majirani kulalamikia harufu kali toka nyumbani kwake.

Kichanga alichokiiba kilinusurika maisha yake na kiliwahishwa hospitali kwa matibabu zaidi.

VIDEO YA BIBI KIZEE ALIYE MALIZA ELIMU YAKE AKIWA NA MIAKA 94


Elimu haina mwisho wala umri, hivyo ndivyo alivyothibitisha bibi wa Marekani mwenye umri wa miaka 94 mwenye wajukuu na vitukuu 41 ambaye mwishoni mwa wiki alisherehekea kumaliza elimu ya shahada ya kwanza na kuwa kikongwe wa pili duniani kumaliza elimu ya juu.
Bibi Hazel Soares, mwenye umri wa miaka 94 wa Oakland, Marekani alikuwa miongoni mwa wanafunzi 500 waliotunukiwa shahada mbalimbali za chuo kikuu.

"Imenichukua muda mrefu sana kumaliza digrii kwakuwa nilikuwa bize sana kwenye maisha yangu",alisema Soares ambaye sasa anamiliki digrii ya Art history.

Soares, ana watoto sita na wajukuu na vitukuu wapatao 40, anashika nafasi ya pili duniani kwa kumaliza digrii akiwa na umri mkubwa sana.

Nola Ochs wa Kansas ndiye anayeshikilia rekodi ya kumaliza digrii akiwa na umri mkubwa kuliko watu wote duniani. Alitunukiwa digrii miaka mitatu iliyopita baada ya kumaliza masomo yake kwenye chuo kikuu cha Fort Hays State University wakati huo akiwa na umri wa miaka 95.

Chini ni VIDEO ya bibi Hazel siku alipomaliza masomo yake.

ASKARI POLISI 5 WA KITUO CHA OYSTERBAY MBARONI KWA KUUA


ASKARI polisi watano wa Kituo cha Oysterbay cha jijini Dar es Salaam, wametiwa mbaroni kwa kuhusishwa na kifo cha Octavian Kashita (38) kilichotokea Jumapili wiki iiyopita aliyedaiwa kuhusika katika tukio la utekaji
Askari hao wamekamatwa na jeshi la polisi nchini wakituhumiwa kusababisha kifo cha raia huyo katika mapambano dhidi yao.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa, tukio hilo la mauaji lilitokea juzi katika eneo la Victoria katika nyumba za serikali.

Alisema, polisi hao walikwenda eneo la tukio majira ya saa 1:00 jioni baada ya kupata taarifa kutoka kwa dada wa Bariki aitwae Sia Minja za kutekwa nyara kwa mtu aliyetajwa kwa jina la Bariki Minja.

Kova alieleza kuwa walipofika eneo hilo la tukio walipoelekezwa na huyo dada, waliliona gari aina ya Toyota Prado lenye namba za usajili T 864 BHC ambalo ndilo lililodaiwa kutumiwa na watekaji nyara hao na lkufanikiwa kuwakamata vijana wannne waliosadikiwea kuhusika na tukio hilo.

Alisema walipofanikiwa kuwakamata vijana hao walianza kuwahoji na katika gari hilo walimkuta mateka akiwa ndani ya gari hilo akiwa na watuhumiwa.

Alisema katika mahojiano hayo kulizuka vurugu kubwa kati ya polisi na watuhumiwa hao, na kutokana na vurugu hizo polisi mmoja alifyatua risasi na kumpata mtuhumiwa Octavian na kupoteza maisha papo hapo.

Kamanda Kova alieleza kuwa, katika uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi hilo ulibaini kuwa chanzo cha tukio hilo la utekaji nyara ni ugomvi wa muda mrefu wa kifamilia kati ya familia ya Bariki na familia ya Martha Makishe ambaye ni mzazi mwenzake ambapo walizaa mtoto mmoja.

Uchunguzi huo ulibaini mzozo huo wa kifamilia umefikia kufunguliwa kwa kesi ya madai namba 31 ya mwaka huu, katika Mahakama ya Kinondoni ambapo shauri hilo linahusisha ugomvi kati yao wawili kumtunza mtoto wao aitwaje Kinsley Bariki.

Hata hivyo Kamanda Kova alipotakiwa kutaja majina ya watuhumiwa hao wengine alisema majina hayo hayatwekwa wazi sasa kwa sababu za kipolisi na inaweza ikavuruga upelelezi.

Hata hivyo ilidaiwa katika watuhumiwa hao wanne yumo mwanafamilia ambaye inadaiwa ni mtoto wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Celina Kombani lakini Kamanda Kova hakuthibitisha hilo na kusema ni mwanafamilia tu kutoka katika familia hiyo ya waziri.

AMUUA MKEWE KISHA KUILA NYAMA YAKE



Mwanaume mmoja wa nchini Marekani amehukumiwa kwenda jela miaka 15 baada ya kumuua mkewe kwa kumchoma choma na kisu mara 250 na kisha kula nyama za mapafu yake kabla ya kunywa damu yake mbele ya mtoto wake wa miaka minne.
Mohammad Solaiman alihukumiwa kwenda jela kati ya miaka 15 na kifungo cha maisha kwa kumuua kikatili mkewe Shahida Sultanna ndani ya nyumba yao mjini New York katika tukio lililotokea mwaka 2007.

Binti yao mwenye umri wa miaka minne alikuwa chumba cha pili wakati baba yake alipokuwa akimuua mama yake na alishuhudia kitendo cha baba yake akinywa damu ya mama yake.

"Alichukua maini na mapafu yake na kuyatafuna", alisema dada wa marehemu na kuongeza "Alikunywa damu yake, binti yake ameniambia".

Wakili wa Solaiman, John Scarpa alikanusha madai ya Solaiman kumgeuza asusa mkewe ingawa alikubali kumuua mkewe.

Wakili huyo aliendelea kusema kuwa Solaiman alikuwa akipigwa na kunyanywaswa sana na mkewe na hiyo ndio sababu iliyompelekea kufanya mauaji.

Akitoa hukumu ya kesi hiyo, jaji Richard Buchter alisema kuwa faili la mshtakiwa halikusema chochote kama alikuwa akinyanywaswa na mkewe.

"Tunachojua ni kwamba, mshtakiwa alimchoma na kisu mkewe usoni, shingoni, tumboni, mgomgoni na kwenye maeneo yake ya siri", jaji Buchter alisema.

"Kuthibitisha kitendo chake cha kikatili alimuonyesha binti yake wa miaka minne mabaki ya mwili wa mama yake", aliongeza jaji Buchter.

Solaiman alihukumiwa kwenda jela kati ya kifungo cha miaka 15 na kifungo cha maisha baada ya kukiri kufanya mauaji hayo.

AFARIKI DUNIA BAADA YA KUIONA MAITI YA AJALI YA NDEGE LIBYA



Afisa mmoja wa Libya amefariki baada ya kuona maiti za ajali ya ndege wakati alipokimbilia kwenye eneo la tukio kutoa msaada.
Afisa huyo ambaye ni mlinzi kwenye uwanja wa ndege alifariki baada ya kuona maiti za watu 102 waliokuwemo kwenye ndege ya Libya ambayo ililipuka wakati wa kutua kwenye uwanja wa ndege wa Tripoli.

Taarifa zinasema kuwa mlinzi huyo alikimbilia kwenye eneo la ajali kwa nia ya kutoa msaada lakini alipofika na kuziona maiti zikiwa zimezagaa kila kona ugonjwa wake wa kisukari ulimzidia na hapo hapo aliiaga dunia.

Taarifa zaidi kuhusiana na kifo chake hazikutolewa ingawa taarifa zilisema kuwa mlinzi huyo alikuwa ni mzee.

Wakati huo huo mtu pekee aliyenusurika kwenye ajali hiyo mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka tisa, Ruben, amesafirishwa leo kurudishwa kwao Uholanzi.

Ruben alikuwa na baba yake, mama yake pamoja na kaka yake mwenye umri wa miaka 11 kwenye ndege hiyo lakini wote walifariki kwenye ajali hiyo.

Ruben na wazazi wake pamoja na kaka yake walikuwa likizo nchini Afrika Kusini kusherehekea ndoa ya wazazi wake kutimiza mwaka mmoja.

Shangazi na mjomba wake toka Uholanzi walikimbilia mjini Tripoli kuwa karibu na mtoto huyo ambaye alikuwa akipatiwa matibabu kutokana na majeraha kadhaa kwenye miguu yake.

Mtoto huyo ameishaambiwa na shangazi yake kuwa wazazi wake na kaka yake wamefariki kwenye ajali hiyo mbaya ya ndege.

AITELEKEZA FAMILIA YAKE BAADA YA KUFANYIWA LIMBWATA NA MTOTO WA KITANGA

MWANAUME mmoja [40] [jina kapuni] mkazi wa Mabibo Jeshini ,amekiri kuwa amefanyiwa mambo anayohisi ni ya kumpumbaza akili na kujikuta akikimbia familia yake na kuhamia kwa msichana mwenye asili ya kitanga bila kujitambua.
Akiongea na mwandishi wa habari hii kwenye mazungumzo ya urafiki, amekiri kuwa inawezekana amefanyiwa kitu mbaya na msichana ambaye hakumtaja jina na kumsahau mke wake na watoto na kwenda kuhamia kwa dada huyo.

Alidai kuwa alipoanza urafiki na dada huyo miezi minane nyuma alikuwa yupo katika hali ya kawaida, lakini ipipotimia kiezi mitano ya urafiki wao alijikuta akiingia katika penzi zito na dada huyo hali ambayo ilimfanya aanze kusahau kidogokidogo familia yake bila kujitambua.

Alidai kuwa alikuwa akienda kwa dada huyo na kuchelewa kurudi nyumbani kwake, mara alijikuta akishindwa kurudi kabisa nyumbani kwake na kulala hukohuko na kumpigia mke wake simu kuwa alikuwa yuko bize kazini na kurudi kesho yake.

Alisema mbaya zaidi alijiona kama yuko tofauti na kuanza kumuona mke wake kama mtu wa kawaida na kumuona dada huyo kama ni mke wake na kuona kamda kitu cha kawaida.

Kutokana na hali hiyo ya kuzidi kusahau familia yake alidai mke wake alikwenda kuripoti kwa ndugu zake yeye na kuulizwa na kukana kuwa si kweli.

Hivyo kadri siku zilivyozidi kwenda hali ndiyo ilizidi kuongezeka ya kusahau familia yake na mke wake kuwataka baadhi ya ya shemeji zake wafike nyumbani kwake walale ili wathibitishe maneno ambayo alikuwa akiwaambia ya kuwa mume wake alikuwa harudi nyumbani.

Shemeji zake hao walithibitisha tukio hilo na kuanza kulifanyia kazi susala hilo na kumfatilia ndugu yao huyo na kugundua kuwa alikuwa akizuzuliwa na mwanamke huyo.

KWa kuwa alikuwa hajitambui ilibidi ndugu hao wamkanye na kumtaka aachane na mwanamke huyo nay eye kukiri ni kweli alikuwa na mahusiano na huyo dada na kuwambia alikuwa anatamani aondokane na hali hiyo lakini alikuwa anashindwa kujinasua kuachana na huyo dada.

“yaani rafiki yangu inawezekana nimeshalishwa limbwata na yule dada kama watu wanavyosema, yaani nimefikia hatua sirudi nyumbani kwangu hii kali? Alisema kaka huyo kwenye mazungumzo na mwandishi wa habari hii

“Na sitamani kumuacha, nimewaambia ndugu zangu mwenye kujua dawa ya kunifanya nirudi nyumbani kwangu anitafutie anipe ili nisisahau kurudi nyumbani kwangu nikienda kwa yule dada, nampenda mkewangu ila ndio hali imenikuta hii” alidai

Monday, May 10, 2010

WATU WATANO WAFARIKI BAADA YA LORI KUTEKETEA KWA MOTO



WATU watano wamefariki dunia baada ya malori mawili yaliyokuwa yamebeba mafuta na betri kulipuka baada ya kugongana huko eneo la Vigwaza Kibaoni mkoni Pwani.
Ajali hiyo mbaya iliyosabaabisha mafgari matatu kuwaka moto na kutekekteza watu hao ilitokea jana katika barabara ya Morogoro, majira ya saa 8 usiku.

Katika eneo la tukio ilidaiwa lori la mafuta lililigonga kwa nyuma gari jingine lililokuwa limeegeshwa pembeni ya barabara kwa ajili ya matengenezo na kusababisha moto mkubwa kuwaka hapo.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Absaloom Mwakyoma alisema ajali hiyo ilihusisha malori mawili aina ya Scania, moja ambalo lilikuwa na trela na ambalo lilibeba mafuta liligonga kwa nyuma lori ambalo lilikuwa limesheheni mzigo wa betri za redio mali ya Said Daniel, mfanyabishara wa Lubumbashi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Alisema wakati moto huo unalipuka chini ya lori alikuwepo utingo wa gari ambalo lilikuwa katika matengenezo Omary Mumbi, mkazi wa Buguruni, alikuwepo dereva wa gari hilo Adam Amulike[ 35], mkazi wa Temeke na dereva mwingine aliyefika kusaidia kutengeneza gari hilo na wote hao waliteketea kwa moto huo

Pia katika ajali hiyo ulimuunguza dereva na utingo wa lori lililosababisha ajali, ambao majina yao hayakuweza kupatikana wote waliteketea kabisa wakiwa ndani ya gari lao.

Alisema wakati moto huo unaendelea kuwaka magari yalisimama na kutoendela na safari lakini lori jingine aina ya Scania lililokuwa na trela lenye tanki ambalo halikuwa na mafuta lilifanya ubinshi kujaribu kupita eneo hilo na baadae kushindwa kuendela na safari baada ya moto kushika kwenye gari hilo na matairi matano ya upande wa kulia kuungua.

MWANAMKE ALIYE WAUA WATOTO WAKE AFIKISHWA MAHAKAMANI

MWANAMKE Benedicto Thadei [44] anayedaiwa kuwaua watoto wake watatu kwa kutumia shoka jana alifikishwa katika mahakama ya mjini Moshi kujibu mashitaka matatu ya mauaji ya kukusudia.
Mwanamke huyo alifikishwa katika mahakama hiyo akiwa chini ya ulinzi polisi na kusomewa mashitaka yake mbele ya hakimu Mfawidhi Simon Kobero wa Mkoa wa Kilimanjaro.


Kwa upande wa mashitaka uliongozwa na Wakili wa serikali, Abdalah Chavulla,alidai kuwa Aprili 29 mwaka huu, majira ya saa 1:30 asubuhi, mshitakiwa aliwaua watoto wake Rose Thadei [12] Noel Thadei[5] na Anthony Thadei mwenye umri wa miaka miwili na nusu na .


Alisai kosa hilo ni kinyumecha sheria cha kifungu namba 196 cha kanuni ya adhabu ambacho kinataja adhabu ni kunyongwa hadi kufa iwapo mshtakiwa atapatikana na hatia.



Hata hivyo mshitakiwa huyo hakutakiwa kujibu chochote mahakamani hapo kama ni kweli alihusika ama la, kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashitaka ya mauaji na kutakiwa kwenda kujibu mashitaka hayo Mahakama Kuu pindi utaratibu wa kimahakama utakapokamilika.


Ilidaiwa na Chavula kuwa wakati mama huyo anafikishwa mahakmani hapo mtoto wake aliyemjeruhi Paschal Thadei[ 9], ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili alikuwa amelazwa chumba cha wagonjwa mahuti katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na tayari madaktari wea hopspitali hiyo walilazika kumfanyia upasuaji wa kichwa kutokana na majeraha mabaya aliyoyapata wakati wa tukio.

Kesi hiyo imepangwa tena kurudishwa mahakamani hapo Mei 19, mwaka huu, kwa kutajwa.

VIDEO YA GAIDI WA NIGERIA FAROUK ABDULMUTALLAN AKIFANYA MAZOEZI YATOLEWA


Video imetolewa ikimuonyesha mwanafunzi wa Nigeria anayetuhumiwa kujaribu kuilipua ndege ya Marekani siku ya krismasi, akifanya mazoezi na wenzake kwenye kambi ya Al-Qaeda nchini Yemen.
Video hiyo inamuonyesha Umar Farouk Abdulmutallab na wanaume wengine wakifanya mazoezi ya kulenga shabaha kwenye kambi ya kundi la Al-Qaeda nchini Yemen linalojulikana kama "Agap".

Umar anakabiliwa na mashtaka ya kujaribu kuiangusha ndege ya Marekani kwa kutumia mabomu aliyoyaficha kwenye chupi yake.

Jaribio lake lilifeli na Umar alibaki na majeraha ya kuungua na moto kwenye sehemu zake za siri.

Alikanusha madai ya kesi zote alizofunguliwa lakini shirika la ujasusi la Marekani limesema kuwa anaonyesha ushirikiano kwa maafisa wa upelelezi.

Umar mwenye umri wa miaka 23 aliwaambia wapelelezi wa Marekani kuwa alipewa mafunzo nchini Yemen. Alipewa vifaa vyenye uwezo wa kusababisha mlipuko mkubwa na kuambiwa nini anatakiwa afanye.

Umar aliwaonya Wamarekani kuwa mamia ya vijana kama yeye wapo wengi nchini Yemen wakipatiwa mafunzo na wako tayari kufanya mashambulizi wakati wowote.

Katika video iliyotolewa, Umar anaonekana akiwa ameshika bunduki na mwishoni mwa video anaonekana akitoa ujumbe katika lugha ya kiarabu.

Haijajulikana ni lini video hii ilitengenezwa na kama ni feki au la.

Chini VIDEO hiyo.

AMJERUHI MMEWE KISA HARIDHISHWI NA HUDUMA KITANDANI


Mwanamke wa nchini Marekani ambaye hakuridhishwa na pafomansi ya mumewe kitandani anashikiliwa na polisi kwa kumjeruhi mumewe kwa mkasi.
Michelle Thomas, 26, alikamatwa jumanne wiki iliyopita baada ya polisi kuitwa kwenye nyumba yao kwenye majira ya saa saba usiku.

Tukio hilo lilitokea Texas, Marekani wakati Michelle alipokasirishwa na uwezo mdogo ulioonyeshwa na mumewe kitandani siku hiyo.

Mume wa Michelle aliwaambia polisi kuwa Michelle alipatwa na hasira baada ya gemu la malavidavi kuisha bila ya Michelle kuridhishwa kimapenzi.

Alisema kuwa Michelle alichukua mkasi na kuutumia kumkatakata kwenye sehemu mbalimbali za mwili wake.

Polisi walimkuta mume wa Michelle akiwa na majeraha makubwa kifuani, mkononi na miguuni.

Michelle amefunguliwa mashtaka ya kudhuru mwili kwa kutumia silaha hatari ingawa mumewe hakutaka kufungua kesi dhidi yake, liliripoti gazeti la Lufkin Daily News.

Michelle huenda akatupwa jela miaka 20 iwapo atapatikana na hatia.

Thursday, May 6, 2010

VIDEO YA WATU KUKAA UCHI ETI NI SANAA HUKO MAJUU


Hii nayo inaitwa sanaa huko majuu, mamia ya watu wanawake kwa wanaume nchini AUSTRALLIA wamejitolea kukaa uchi kwenye sehemu ya hadhara ili kupiga picha za sanaa kwaajili ya jumba la makumbusho.
Katika kusherehekea miaka 10 ya jumba la sanaa la OPHRA mamia ya watu wanawake kwa wanaume walikusanyika kwenye bustani wakiwa uchi wa mnyama kwaajili ya kupiga picha za sanaa.

Mpiga picha wa Kimarekani, Spencer Tunick alifanikiwa kuwakusanya mamia ya watu ambao waliamua kubakia na suti zao walizozaliwa nazo wakipangwa katika staili mbalimbali ili kutengeneza picha za maumbile tofauti tofauti.

Inakadiriwa kuwa watu 5,000 wazee kwa vijana walishiriki katika zoezi hilo.

Angalia video hii chini ujionee mwenyewe hali ilivyokuwa.

KIKWETE: MSIPONIPA KURA WENGINE WATANIPA


Hii ni moja kati ya kauli alizozitoa Rais Kikwete wakati wa hotuba yake aliyoitoa juzi jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na wazee kjatika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Rais alitoa kauli hiyo baada ya kuonekana kukerwa na viongozi wa Tucta wanaoandaa mgomo nchi nzima.

“ Mgomo huo una lengo la kuongezewa mshahara tu au kuna lingine? Alihoji rais, mimi naona mnataka kuninyima kura zenu, basi kama mmepanga hivyo mninyime tu, wengine watanipa” alisema Rais

“Mana sitaki kuwaongopea kuwa tutalipa kima hicho kama mnataka kugoma na mshahara huo kama hatutawapa basi, ninyimeni kura zenu wengine watanipigia” alisema

Pia aliwasihi wafanyakazi hao atakayegoma atakuwa amejifukuzisha kazi na kukosa haki yake ya msingi katika miaka yake aliyoitumika serikali.

Pia alisema kwa yeyote atakayefika kazini na akae na asiendelee na kazi pia atakuwa amejifukuzisha mwenyewe na hakutakuwa na msamaha na atakayethubutu kuandamana sheria itafata mkondo wake.

UTARATIBU MPYA WA KUOMBA VISA YA MAREKANI

UBALOZI wa Marekani nchini umetoa utaratibu wa maombi ya viza kwa kutumia fomu mpya za DS -160 kwa ajili ya maombi ya muda mfupi utakaoanza kutumika Mei 31, mwaka huu.
Taarifa ya balozi hiyo iliyotolewa kwenye vyombo vya habari, ilieleza kuwa waombaji wote wa viza za muda mfupi watatakiwa kujaza fomu za DS-160 zitakazopatikana kwa njia ya mtandao.

Ilisema waombaji wote wanashauriwa kuanza kutumia fomu hizo mpya bila kuchelewa ili waweze kupata viza zao.

Taarifa hiyo ilielezea kuwa Idara ya Uhamiaji na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, imeboresha fomu za DS-160 kwa waombaji wote wa viza za muda mfupi (NIV) ili kuleta mabadiliko katika fomu zinazopatikana kwenye mtandao (EVAF).

Taarifa hiyo ilisema kwua tofauti inayopatikana kwenye fomu za DS-160 ipo kwenye hatua ya kwanza ya maombi ambapo wanatakiwa kujaza kupitia mtandao.

Tovuti ambayo utaweza kupata fomu za DS-160 kwa maelezo ya hatua kwa hatua ni http://www.tanzania.usembassy.gov au wataweza kuwasiliana na Idara ya Uhamiaji kwa barua pepe: drsniv@state.gov ama kutembelea katika ofisi za balozi.

RAIS WA NIGERIA AFARIKI DUNIA



Rais wa Nigeria Umaru Yar'Adua pichani amefariki dunia Thursday, May 06, 2010 3:48 AM
Rais wa Nigeria, Alhaji Umaru Yar'Adua ambaye kiti chake cha urais kimekuwa kikikaliwa na makamu wake kwa miezi kadhaa sasa baada ya rais huyo kuugua ugonjwa wa moyo, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 58.
Kwa mujibu wa msemaji wa rais huyo ambaye hakutaka kutaja jina lake wakati akiongea na shirika la habari la BBC, alisema kwamba rais Yar'Adua amefariki dunia jana jumatano ingawa serikali ya Nigeria bado haijatoa taarifa rasmi.

Rais Yar'Adua alichaguliwa kuwa rais mwaka 2007 lakini kutokana na matatizo ya moyo na figo hajaonekana kwa wananchi wake kwa miezi kadhaa.

Baada ya rais huyo kuugua muda mrefu huku akipatiwa matibabu nchini Saudi Arabia, hatimaye makamu wa rais, Goodluck Jonathan aliteuliwa kushikilia nafasi yake mpaka rais huyo atakapopona.

Taarifa zinasema kuwa rais huyo aliiaga dunia jana jumatano kwenye villa lake nchini Nigeria kwenye majira ya kati ya saa tatu na saa nne usiku kwa saa za Tanzania.

Yar'Adua alienda Jeddah, Saudi Arabia kwaajili ya matibabu mwezi Novemba mwaka jana na alitumia miezi mingi sana huko kiasi cha wapinzani wake na viongozi wa zamani wa Nigeria kumshauri ajiuzulu.

Wakati huo Yar'Adua alimkabidhi mikoba ya urais makamu wake, Goodluck Jonathan lakini hata aliporudi toka Saudi Arabia mwezi februari mwaka huu, Goodluck Jonathan aliendelea kukikalia kiti cha urais.

Taarifa zinasema kuwa baada ya kufariki kwa rais Yar'Adua, makamu wake wa rais ataapishwa rasmi kuwa rais katika siku zijazo.