Monday, April 12, 2010
NAKAYA SUMARI AJIUNGA NA CHADEMA
MSANII mahiri wa muziki wa kizazi kipya hapa nchini, Nakaaya Sumari jana alitangaza rasmi kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akiwa na nia ya kuwahamasisha vijana kujitambua zaidi na kutetea haki zao za msingi na demokrasia kwa ujumla.
Mwanamuziki huyo wa kike, aliyewashangaza watu wengi mkoani hapa kwa kuwa wa kwanza kujiingiza katika masuala ya kisiasa, bila kuhofia ama kuogopa kazi zake zinaweza kushuka kiwango, alisema, ataweza kuendesha shughuli zake za muziki na siasa pia.
Nakaaya alijiunga mapema jana mkoani hapa, mbele ya waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali na kusema kuwa kwa muda mrefu alikuwa na kiu kubwa ya kujiunga katika chama cha siasa chenye mwelekeo, dira na nia nzuri ya kusaidia wananchi wake, ambapo aliona CHADEMA ndicho chama pekee ambacho kinaweza kutimiza ndoto zake za kujiingiza katika masuala ya siasa.
“Kwa kipindi cha muda mrefu nimekuwa na kiu ya kujiingiza katika siasa, ili kuweza kuwahamasisha vijana wa Kitanzania kujitambua na kutetea haki zao za msingi, hasa kwa demokrasia bila kununuliwa ama kushurutishwa na vyama, ambavyo havina msaada wowote katika maisha yao,” alisema Sumari.
Alisema, kutokana na Tanzania kuwa na vivutio vya kutosha, kuwawezesha wananchi wake wote kuondokana na umaskini, lakini hadi hivi sasa, anashangazwa na chama kilichopo madarakani kushindwa kutatua shida na adha kubwa ya umaskini zinazowakumba Watanzania, ambao wengi wao ni maskini.
“Nchi yetu ina rasilimali za kutosha kabisa, hasa kwa upande wa madini ya Tanzanite ambayo yatosha kuwawezesha wananchi wote kuwa katika kiwango bora na kinachostahili kimaisha, mbali na vivutio vingine vya kitalii vilivyopo, lakini cha kushangaza mpaka hivi sasa, wapo Watanzania ambao wanaishi katika hali duni kimaisha na chini ya dola moja kwa siku,” alisema.
Alisema, amejiunga na chama hicho hivi sasa na si mwaka jana ama mwaka juzi, kutokana na kuona hivi sasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu nchini Tanzania, jamii itamhitaji zaidi katika kuwahamasisha juu ya kujitambua katika haki zao za msingi, hasa katika masuala ya kisiasa.
Vyombo vya habari vilimhoji mwanadada huyo kwa nini katika hatua za kwanza kwa lengo lake la kuamua kuingia katika siasa, ameamua kujiunga na chama hicho badala ya kuingia Chama tawala (CCM), au Chama cha Jamii (CCJ), alijibu kwa mshangao kuwa hajaona kama ni vyama ambavyo vipo kwa ajili ya kusaidia watu, bali ni kwa maslahi yao binafsi.
Nao viongozi wa chama hicho mkoa, waliupongeza uamuzi wa msanii huyo kwa uthubutu wake wa kujiunga katika masula ya siasa bila woga wa aina yoyote ile, huku wakimuahidi kumruhusu kugombea nafasi yoyote ile ya uongozi, pindi atakapotimiza masharti na taratibu zote ndani ya chama.
Viongozi hao walimkabidhi kadi ya uanachama na kumtaka kuwa makini sana, hasa katika kuhamasisha vijana wenzake, huku akiwashawishi wasanii wengine kuingia katika siasa na kuongea yale yote yanayostahili kwa haki kwa manufaa ya nchi yao.
"Ukiwa kama kijana mdogo sana na msanii ambaye ni kioo cha jamii, tunataka tuone bidii yako ya kuweza kufichua na kukemea maovu yote, utakayoyaona ndani ya vuguvugu la kisiasa ndani ya nchi yetu, ili jamii nayo iwe na imani na wanasiasa wake," alisema mmoja wa viongozi hao wa CHADEMA.
Aidha, waliwataka wasanii wote nchini ambao wana uchungu wa kweli katika nchi yao, kujiunga kwa wingi katika chama hicho, ili kuweza kufikia na kutimiza lengo la kuwakomboa wananchi walio wengi masikini na sauti za wanyonge kusikika, hasa katika suala zima la kutatua matatizo yao ikiwa ni pamoja na umaskini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment