WALIMU wawili wa Shule ya Msingi ya Tarangire mkoani Manyara, Joyce Paulo, 30, na Anna Nkya, 24, wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kutokana na kilekilichoelezwa kuwa niugomvi wa mapenzi.
Imeelezwa kuwa askari aliyefanya mauaji hayo alikuwa lindoni kwenye hifadhi hiyo, lakini akaamua kuacha kazi yake na kwenda hadi nje ya hifadhi kutekeleza mauaji hayo ya mtu anayesadikiwa kuwa ni mkewe na mgoni wake.
Tukio hilo la aina yake lilitokea juzi saa 3:00 usiku eneo la Tarangire lililo kwenye Kata ya Ngaiti baada askari huyo, ambaye ametajwa kuwa ni Paulo Keregesi kuvamia nyumba waliokuwa wanaishi walimu hao na kuwamiminia risasi zilizokatisha maisha yao.
Diwani wa Kata ya Ngaiti inayopakana na hifadhi hiyo, Olais Ole Koine alisema kabla ya mauaji hayo, Keregesi alikuwa ametengana na mkewe Joyce, ambaye mwalimu na ambaye amezaa naye watoto wawili.
Diwani huyo alisema taarifa ambazo wamepata mara baada ya mauaji hayo zinaeleza kuwa askari huyo na mkewe Joyce ambao wote ni wenyeji wa mkoani Mara walikuwa na ugomvi kwa takriban miezi miwili iliyopita.
Alisema, hata hivyo, walikwenda nyumbani kwao kusuluhishwa lakini waliporudi mwanamke huyo hakurejea kwa mumewe anayeishi ndani ya hifadhi hiyo na akaamua kuishi na mwalimu mwenzake nje ya hifadhi hiyo.
"Baada ya hali hiyo ndio juzi majira ya saa 3:00 usiku askari huyo aliyekuwa lindoni na silaha alivamia nyumba ya walimu na kwa kupitia dirishani aliwapiga risasi na wakafariki papo hapo na baadaye akatoweka," alisema Diwani Koine.
Alisema wamepata taarifa kuwa askari huyo aliyekuwa na bunduki aina ya AK 47 aliiterekeza eneo la Mdori na kukimbia na baadaye alituma ujumbe mfupi wa simu kueleza kuwa anahusika na mauaji hayo na kwamba ameiacha pikipiki mjini Babati.
"Muda huu tunajiandaa kuja Arusha ili kupanga taratibu za kusafirisha marehemu kwani Mwalimu Nkya ni mwenyeji wa Machame na Joyce ni mwenyeji wa Serengeti," alisema Diwani Koine.
Polisi mkoani Manyara wamethibitisha kupokea taarifa za tukio hilo na wanamsaka askari huyo. Mkuu wa hifadhi ya Tarangire, Erastus Lufungulo, ambaye kwa sasa yupo likizo, pia amethibitisha kupata taarifa za mauaji hayo.
"Naomba uwasiliane na mkurugenzi mkuu wa Tanapa kama kuna maelezo mnahitaji kuhusu huyo askari," alisema Lufungulo.
Hata hivyo, meneja uhusiano wa Tanapa, Pascal Shelutete alisema jana kuwa bado hawajapata taarifa kamili za tukio hilo na aliomba kupewa muda zaidi ili atoe maelezo zaidi.
Wednesday, April 28, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment