HATIMAYE Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema amefungua kesi ya madai ya sh bilioni moja dhidi ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta.
Kesi hiyo ya madai namba 32/10 imefunguliwa na mwenyekiti huyo anayeongoza chama chenye wafuasi wasiozidi 500,000 nchini kote kwenye Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari, makao makuu ya chama hicho Magomeni, Dar es Salaam jana, Mrema alieleza dhamira yake ni kutaka kupata uthibitisho kutoka kwa spika huyo wa Bunge kama amefilisika na kwa sasa anahongwa na makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kadhalika, Mrema anadai kwamba kitendo cha Sitta kuieleza jamii kupitia gazeti kwamba amechanganyikiwa na amepewa fedha kwa ajili ya kuipigia debe CCM kina lengo la kumdhoofisha katika kampeni zake za kuwania ubunge wa Vunjo kwa tiketi ya TLP.
“Katika barua niliyopeleka kwa Spika nilitaka aniombe radhi kwa uzito ule ule katika kipindi cha siku saba na kunilipa fidia, lakini akawa kimya kwa muda wote huo,” alisema Mrema na kuongeza kwamba washitakiwa wengine katika kesi hiyo ambayo haijapangiwa jaji ni gazeti lililochapisha habari hiyo na mhariri wake akiamini kuwa ndiyo chombo kilichotumika kumchafua na kumpotezea hadhi aliyojijengea.
“Hivi kweli mimi nimechanganyikiwa? Kwanini anivunjie hadhi yangu?… Nimekuwa Naibu Waziri Mkuu wa nchi hii, nimefanya mengi sana nilipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, kwa miaka 30 nimeitumikia Tanzania,” alisema Mrema.
HABARI NJEMA KWA WAFUGAJI
16 hours ago
No comments:
Post a Comment